Elimu ya Maisha niliyoipata katika Riwaya ya " Haini" ya Mtunzi Adam Shafi.

 


Kuhusu Riwaya

Haini ni riwaya inayochukua tukio la kihistoria  la kuuawa kwa kiongozi wa kiafrika mwaka 1972, na kulifanya kiini cha ya kuyachunguza matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya nchi za kiafrika baada ya uhuru, chini ya mifumo ya utawala inayojali tu maslahi ya wachache.


Ni riwaya yenye uhusivu na taharuki ya kipekee, na licha ya kuwa na sifa za kitanzia, inasheheni msambao wa ucheshi na viliwazo.


Kuhusu Mwandishi

Adam Shafi alizaliwa mjini Zanzibar mwaka 1940, baada ya elimu yake ya shule ya msingi alijiunga na chuo cha ualimu cha Seyyia Khalifa ( sasa chuo cha ualimu cha Nkurumah) mwaka 1957 hadi mwaka 1960.


Alipata diploma ya juu katika fani ya siasa ya uchumi katika fani ya siasa ya uchumi katika chuo cha Fritz Heckert, katika iliyokuwa jamhuri ya kidemokrasia ya ujerumani mwaka 1963.


Alipata mafunzo ya uandishi wa habari mjini Prague, nchini Czechoslovakia (sasa jamhuri ya Czesh), mwaka 1964 hadi mwaka 1965, nchini Sweden mwaka 1982 na nchini Marekani mwaka 1985.


Adam Shafi alikuwa mwenyeketi wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA) kuanzia 1998 hadi 2002. Alichagua kuwa mwenyekiti wa Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania (BAMVITA) mwaka 2002.


Adam shafi ameandika vitabu vyengine zaidi ya vitatu, vikiwa ni riwaya: Kasri ya mwinyi Fuad – ambacho kimetafsiriwa kwa Kifaransa, Kirusi, na Kijerumani; Kuli, Vuta n’kuvute na Mbali na nyumbani.


Utangulizi


Dondoo katika kitabu hiki kimegawanyika katika sehemu tatu ambazo zimenibamba, kunisisimua na kunikosha nafsi yangu; ambapo ni mafunzo ya kimaisha niliyoyapata kitabuni, sehemu zilizonifutia kutokana na umahiri wa muandishi katika namna yake aliyetumia katika kuwasilisha simulizi yake — na ulevi wangu wa mashairi, utenzi na namna vitu vinavyoandikwa katika namna hiyo imenifanya nijuumuishe tenzi zote alizotumia mwandishi na kama alivyotumia ubeti katika wimbo wa marehemu Mzee Baraka Mwinishehe —  “tabia njema ni silaha”


Furahia dondoo zangu;


Mafunzo 19 kitabuni


1) Njaa haina adabu pale inapokushika – wacha kipande cha muhogo hata ukimtupia paka hakifuti, ila hata ufundo unaweza kula.


2) Usingizi nao ukikamata hauna ujanja – ukikushika utalala popote pale, hutajali zogo la mbu wala adha ya kunguni.


3) Gerezani hamna kaburi – utatoka tu; kama hukutoka mzima, itatoka maiti yako.


4) Njaa inaweza ikageuza watu wakawa wanyama kwa matendo yao; wakakogombania chakula  bila ya heshima, bila kujali utu wao – ama kweli njaa hain adabu.


5) Gerezani inawezekana kuwa cha watu kujifunza na kuacha tabia zao mbovu ila gerezani humo humo inaweza ikawa nyumba iliyojaa laana na hizaya na kufanya ikose heshima  na busara; ambayo watu wanaweza kupoteza hisia za utu  na sharafu zao.


6) Gerezani unaweza kukuta rundo la watu mahabithi na wenye utovu wa huruma,


7) Nyimbo mbaya haimbelezei mtoto.


8) Japo adha na mateso ya gerezani; ila wapo wanaofanya vitu huenda vikawa si halali ila vikawaletea tasnifu za raha na utukufu pale walipo katikati maisha ya shida na mateso.


9) Nnachotaka kukuambia ni kwamba ukiwa katika shida usikate tamaa; Hakuna shida inayozaa shida, shida maisha huzaa kheri.


10) Si mkwezi wala si mkulima aliyepata cheo kwa ujabari wake au ukereketwa wake wa kisiasa.


11) Heri kupatikana ndani ya tumbo la shari.


12) Siku zote furaha na kicheko ni ishara  ya matumaini mema.


13) Mauti ukiyatafuta, usiyatafute yatakuja tu. kama hutaki kuyatafuta wewe popote pale ulipo.


14) Kicheko cha mwoga ni kicheko cha utumwa.


16) Heri na ya shari yote yanatokana na Mola.


17 ) Kila litokealo huwa limeshaandikwa na mwenyezi Manani na hakuna awezae kuligeuza.


18) Ukiona panafuka moshi basi ujue pana moto.


18) Kheri inaletwa na Mungu ni shari inaletwa na Mungu.


19) Karl Marx alisema dini ni kasumba ya binadamu.





Dondoo Kitabuni


… hawapo duniani tukasema wanaishi, wala hawapo akhera tukasema wamekufa…


… mwili mzima unamuuma, hana hata sehemu moja ya mwili  wake iliyo na afadhalli, mahamum mahututi… 


… lakini vicheko vyao viliwatia wale walio vyumbani kiwewe, wakijua kwamba saa imefika , saa ya mateso na idhilali… 


… sisi tushasema , asiyekuwemo haingii na aliyekuwemo hatoki, tutachagua barabara mchele,chenga, chelele na chua… 


… “ama kweli nguo ya kuazima haisitiri matako”...


…. Kwa Hamza wali ule ulikuwa si chochote si lolote. Ni bondo tu lililochemshwa msege mnenge ili mahuluki wa gereza lile wajaze matumbo yao.


… wafanyakazi wa humo huchaguliwa kwa tahadhari kubwa na lazima wawe na sifa ya  utovu wa utu na umaskini wa huruma , uhabithi na ukatili… 


… Ambar alimtazama. Haamini kama kweli Sururu ameazimia kujitosa katika janga jengine. “ Naona ile ngazi itakuponza. Haya masaibu yaliyo kwisha tufika si madogo, wewe sasa unatafuta mengine, hebu fanya subira, uwe mtu mzima. Usikubali kuyapa nguvu  mawazo ya kijahili” – alimuambia sururu… 


… kwako wewe ni mawazo ya kijahili, kwangu mimi ni mawazo ya kiakili. Kwaheri mimi nakwenda zangu… 


… unakopa mwanangu halafu uje ulipe nini? Hali yenyewe ndio kama hii. Usikope mwanangu ukadharirika biure! Majirani wakaanza kututia  mdomoni . kwanza si vizuri mtoto wa kiungwana kuchuna uso kwenda kumkopa mtu usiyemjua…


… starehe yote waliokuwa nayo ndani ya chumba kile, hakuna hata mmoja aliyediriki kutia nyama akanennepa. Walibakia vifefe, wamekonda ni mafupa matupu. Kwao ile ilikuwa ni starehe ya mbwa tu, kukulia mkia wake…


… wamekuwa kama anayeomba pepo, hafiki huko peponi mpaka afe, wao wanaomba nusura, watoke katika mtego waliotegewa. Hawawezi kunasuka mpaka wanase kwanza.


… joto la hofu limewapanda unafukuta ndani ya miili yao, wote wameshikwa na maumivu ya roho zilizojaa wasiwasi. Deko waliokua wakilipata kwa kubembelezwa na kulishwa vinono limekwisha, wamewageukia ghafla, usuhuba haupo tena, sasa ubaya ubaya tu.

… mategemeo yao yote ya uhai yamepeperushwa na upepo wa balaa na hali ya kukata tamaa ilionekana katika nyuso zao. Wingu la kiza lilitanda mbele yao na ile ishara ya nusura hawaioni tena imemezwa na wingu lile la nakama…


… kelele zao zikavuma pale uwandani, wote wamepiga magoti, vichwa wameniweka upande, viganja vya mikono wamevinyanyua juu, wanaomba unyenyekevu nusura ya roho zao. Milango ya mbinguni ilikuwa iwazi, dua walizokuwa wakiziomba zitakabaliwa nusura waliyokuwa wakiomba ikawashukukia palepale uwandani…


… amevaa suti nzuri ya lasi na tai ameikaza shingoni, anameremeta, mweupe kama suriama wa Mzungu na Mwarabu. Nywele zake za singa kazichana vizuri kwa kuzirudisha nyuma zikafanya mawimbi ya mchanganyiko wa mvi na nywele nyeusi.


… Uchungu uliotumbuka ndani ya moyo wake kwa yale aliyoyasikia ulizidi uchungu wa ile kahawa aliyokaribishiwa na Ali Mabunye. Mwili ulimyong’onyea oho ikanyonga na ule unyonge alioishi nao kwa muda mrefu ukazidi lakini alisaidiwa na ule ucha Mungu wake tu na imani yake kwamba ya heri na ya shari yote yanatokea na Mola, ‘ Subhana azza wa jalla...


… chumba kile amacho kila siku hujaa dua za kuwaombea watu heri, afya uzima na mafanikio, pale watu hao wanapokuja kuombewa na Mzee Maftah, Mungu awaondolee dhiki na shida zao, leo kimejaa dhiki na shida zilizomkumba yeye maftah mwenyewe. Hana raha, hana chochote anachokiona mle chumbani isipokuwa udhia tu na majonzi yaliyomjaa moyoni.


… usingizi mwepesi ulimchukua ghafula, akalala. Usingizi wenyewe ulikuwa wa juu juu tu, kama mtu aliyeshikwa na maruemarue, hayupo macho na usingizini hayumo.


…” Basi kama wewe unaomba shari hiyo shari iwe yako pekee yako” alisema Mfaume, kahamaki… “na wewe kama unaomba kheri basi hiyo kheri iwe yetu sote”, Hamza naye akamwambia Mfaume kwa sauti ya stihizai.


… Sururu aliinua macho juu akaangalia mawinguni, akamwona ndege akinyinyirika, mbawa amezitandaza anaelea hewani, yuko huru, hakuna wa kumtia msukosuko wa maisha yake… una maana gani ubinadamu wake ikiwa ubinadamu wenyewe umekubwa na dhiki na idhilali, hauna thamani yoyote.


… yana maana gani maisha ikiwa maisha yenyewe yamo katika mateso yasiyokuwa na mwisho? Maisha yasiyokuwa na heshima anayostahili binadamu.



hakuna hata mmoja aliyekunywa  ule uji kwa raha, ikiwa chakula cha jela kina raha yeyote…


… chuki dhidi ya ilijazwa ndani ya nyoyo za watu ikijaa tele ikiwa ishara yoyote ya kuwaonea huruma ni usaliti mkubwa… 


…Huruma huonewa anayestahili kuonewa huruma. Hata Mungu humpa adhabu kali kiumbe aliyemuumba yeye mwenyewe pindi kiumbe huyo akimkosea…


…Wake wa washatakiwa hujazana hapo na watoto wao, ndugu na jamaa hufika kila siku ya kesi, wambeya na wazabizabina wanaotaka kuduhushi mambo yasiyo wahusu, naa pia hujaa tele hapo…


…”kiongozi wa makoministi, Karl Marx alisema dini ni kasumba ya binadamu, wewe unakubaliana na hayo?”... “ Karl Marx aliposema dini ni kasumba ya binadamu, viongozi wa dini wakati huo walikuwa wakishirikiana na  mamwinyi na mabepari kuwakandamiza wafanyakazi  na wakulima”.


… “ wacha ufidhuli! Jibu ninavyokuuliza!”

“Ndiyo mimi mwanajeshi”

“Siku ya mauaji, saa ya mauji, wewe ulikuwa wapi?”

“Nilikuwa kwetu”

“Kwenu ulikwenda kufanya nini?”

“Ala! Unaniuliza kwetu nilikwenda kufanya nini? Kwani  mtu kwao huenda kufanya nini” Heri naye akauliza….


“Mwongo!” Chopra alipiga kelele.

“ A-aaa. Bwana Chopra usinipigie kelele, mimi si kiziwi, ukisema taratibu nitakusikia”… watu wote katika ule ukumbi wa mahakama wakaangua kicheko, wakacheka.


“Chopra  alimtazama Heri kwa hasira, unatamani amrukie pale kizimbani amkabe roho, amebadilika rangi, ameiva amekuwa mwekundu kama papai, jasho linatoka, hana la lusema… “ wewe ni haini tu!” Chopra alimwambia Heri.


“ Bwana Chopra wewe ni hakimu, Mahakimu wale pale”  Heri alionesha kidole kile kwenye jukwaa. “ wao ndio watakaotoa hukumu na kusema kama mimi ni haini au si haini” – alisema  Heri kwa utaratibu.

 

“ Bwana Chopra anadhani mwenye kuyaona maisha matamu ni yeye tu na sisi sote maisha yetu si chochote si lolote, ni watu  wa kutoswa baharini tu, tena kwa kutupwa kutoka kwenye helikopta. Mungu atunusuru na hilo!” Aliendelea Hamza.


Na hamza naye akamtazama Chopra, macho yao yakakutana, lakini wakati macho ya Chopra yalikuwa yamejaa hasira, ya Hamza yalijaa busara.


“ una heshimu msahafu na wewe kila siku nakukuta Starehe Club unalewa”

“Kwani wewe Bwana Chopra unapokuja starehe club huwa unakuja kusali?”.... Chopra akaduwaa, hana la kujibu na mara hii badala ya kukasirika, alicheka, akarudi juu ya kiti chake akakaa.


…Usiku kucha wanaweza kama mbele yao kuna kheri au shari. Heri ndiyo wanayoiomba , shari ndiyo wanayoiona… 


Leo Chopra amevaa suti nyeusi na tai nyeusi, siyo kwa sababu vaa hilo huvaliwa na mawakili wanapokuwa mahakamani bali kwa sababu ya kuwapa ishara washtakiwa kwamba msiba mkubwa unawasubiri, wao na walio wao wote.


…Punda hendi ila kwa mikwaju na washtakiwa wale ilibidi wapigwe mikwaju kama punda ili waseme ukweli.


…Hamza alimtazama Chopra na Chopra naye akamtazama Hamza, macho yao yakakutana. Hamza, macho yao yakakutana. Hamza akasema mouoni mwake “ Hunipati ng’o.”..


   

   

  Tenzi 


1)

Nilipochukua mimba,

Taabu na mashaka yangu.

Usiku kucha silali,

Nawania roho yangu.

Nambiwa mwana si wangu,

Mwana ni wa mume wangu.


Kile kidau kijacho

Hamkosi mna chungu

Mna mkufu nitunge

Kadiri ya shingo yangu

Hiupata siuvai

Wala simpi mwenzangu

Nenda mpa mama yangu

Msiri wa mambo yangu,


Kua mwanangu ukue

Kua nikupe wasia

Nikupe kundi la ng’ombe

La  mbuzi unywe maziwa

Kwa mola wako karimu

Nakuombea matatu

Kwanza akupe uzima

Pili akupe na kitu

Tatu upendwe na watu.


Usilie usilie

Ukaniliza na miye

Machozi yako yaweke

Nikifa unililie

Oh! Oh! Oh! Mtoto

Oh! Oh! Oh!


2)… hamza aliliweka lile gamba chini ya kirago akijinyoosha juu yake, mguu aliupachika juu, akipiga miluzi kwa sauti ndogo ile nyimbo aliyekuwa akiipenda;

msegeju ana ng’ombe,

Nami nina ng’ombe zangu.

Namuambia tuchunganye, hataki

Kwaheri na kwenda zangu”...


3)… kitoto kilitabasamu , vijino viwili vimechomoza juu ya ufizi wake wa chini. Hamza alimyanyua, akamrusha juu akamdaka, akamwimbia. 

Pole mwanangu nyamaza

Ukilia waniliza, hoya

Wanikumbusha ukiwa hoya…”


4)…Kondo anaimba na sururu anamwangalia vile mishipa ya shingo ilivyomsimama, amekakamaa utadhani ndiyo Mbaraka Mwinishehe mwenyewe yuko jukwaani akiliporomosha rumba.

“Heshima  kijana, tanguliza kwanza mbele

Ujeuri, mbaya ohoo

Uzuri si hoja, tabia  njema ni silaha

Utapendwa kokote ohoo’”... 


5) … “ Kombowe we kombo

Kanipe mapesa yangu

Kilichonitoa nyumba

Wivu wa mke mwenzangu

Kahamia kianga mselemu”


















    


You Might Also Like

0 #type=(blogger)

Top Categories