Barua kwa Ruge Mutahaba.



Ruge mutahaba nimeandika barua na nipo naisoma kwa ajili yako.
Nilitamani uwepo wako hapa lakini haikujaliwa kuwa hivyo.
Hata hivyo ni wajibu wangu kuandika na kusimulia watu kuhusu wewe.

Barua hii ni mahususi kwa ajili ya kukumbuka makubwa ambayo umewahi kuyafanya.
Wakati wengi wakikumbuka kama mpambanaji kwenye swala la burudani na maudhui ya media ulitubariki
na “ Malaria No More”. Uliifanya nchi yetu na ulimwengu kwa ujumla kujua hitaji lako la kuisaidia nchi yako. Wengi walionufaika katika kipindi hicho ambacho malaria ilikuwa janga kubwa nchini, ulitupa faraja!
Nakumbuka kwa ukaribu hitaji lako la kuisaidia jumuiya ya watanzania kiuchumi ukatizama maeneo na mambo mbalimbali ukagundua wengi bado hawajui nini wafanye.

Uliipenda sana nchi yako pamoja na vijana wake ukaamua kutuletea ‘FURSA’, ulitembea nchi nzima, ukafika kona mbalimbali. Na wanawake, wanaume, mpaka vijana walipata elimu yako.
Uliamua kuwa mwanajeshi wa taifa hili kwenye mapambano ya kiuchumi. Upendo wako kwa Taifa lijalo ulikufanya kuhimiza kwenye mabadiliko na usimamizi wa watoto wetu ukagundua watoto wa kike wanahitaji msukumo wa ziada toka katika ngazi ya nchini.

Huku mengine yote yakiendelea, uliamua kutupatia ‘ KIPEPEO’ programu maalum iliyolenga kuwainua watoto wa kike waliopo mashuleni na kuwafundisha stadi za maisha, huku tukiwandaa na maisha ya kesho ulikuwa uncle wao mzuri sana na walikupenda.

Nafahamu upendo wako kwa mama yako, ulimpenda sana, na ukataka heshima unayompatia basi iwe kwa wanawake wote. Malkia wa Nguvu itaendelea na itabaki kuwa nembo yako inayodumu, wengi wameipita katika tuzo hizi zikawafungulia dunia, na sasa mamia na mamia ni wanufaika na wanaendelea kuishi umalkia wa nguvu katika sekta mbalimbali, uligeuka kuwa kaka na mtoto wao kipenzi, malkia wote wa Tanzania.

Tupo hapa leo tunashuhudia Tanzania yenye mabadiliko makubwa ya usafi wa mazingira. Mboni zako ziliona mbali katika kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanya mambo ya tofauti. ‘Nyumba Ni Choo’ itabaki kuwa moja ya mambo mazuri ambayo ulishirikiana na kuyapa maisha na sasa watanzania wengi wanaishi mahala pasafi.

Ulifika katika hatua iliyotukuka na hata nyumbani kagera wanakukumbuka kila tukitaja Azimio la Kagera ulilolifanya, wapo wanaoniambia ni azimio la jasiri muongoza njia, uliwatendea haki ndugu zako wote nyumbani pale.

Nikuahidi kuwa nitaendelea kuandika barua nyingi kwa ajili yako, yapo mengi ya kusimulia. Leo nitaishia hapa. 
Ulichonga barabara, ukaona haitoshi ukajenga madaraja, bado haikutosha ukaamua kabisa kuwa dereva wa kila mmoja na kutupitisha katika hizi barabara ndiomana ukaitwa jasiri muongoza njia.

Ninakupenda sana!

Mimi Mtanzania.


   




   


You Might Also Like

0 #type=(blogger)

Top Categories