Maji Hayafati Mkondo.

Maji Hayafati Mkondo

 

Maji Hayafuati Mkondo ni riwaya inazaungumzia changamoto anazokumbana nazo mwanamke katika kufikia ndoto za maisha yake. Mama sinta, Sinta na Mercy ni wahusika ambao mwandishi anawatumia katika kuonesha mchango wa mwanamke katika kuijenga familia kimaadili na kiuchumi. 


Wahusika hawa wanachorwa na mwandishi kama wanawake wenye utashi mkubwa wa kupambanua mambo pamoja na ujasiri mkubwa katika kupambana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha yao.


Kwa kutumia wahusika hawa na wengine, mwanishi anasisitiza suala la umuhimu wa wazazi kushiriki kwa pamoja  katika kulea watoto na kuijenga familia kwani ndiyo mhimili wa taifa lenye uadilifu. Mwandishi anapiga vita wazazi na walezi ambao wanashiriki kwa makusudi katika kuangamiza kizazi kipya. 


Anakemea suala la matumizi ya madawa ya kulevya, biashara ya binadamu pamoja na rushwa. Mwandishi anaonesha pia umuhimu wa vyombo vya dola katika kusimamia haki za wanaodhulumiwa katika jamii.


Kuhusu Mwandishi


Dkt Felistas Richard Mahonge ni mwandishi wa kike wa Kitanzania aliyezaliwa katika kijiji cha Mbuzii wilyani Lushoto mkoani Tanga. Amesoma shule za msingi Kitopeni, Hazina na Mhelo wilayani Lushoto kisha akapata elimu ya sekondari shuleni Popatlal Tanga. Alisoma stashahada ya ualimu katika chuo cha Mpwapwa akijikita katika masomo ya lugha ya kingereza na kiswahili. 


Mwaka 2002 alijiunga na Chuo kikuu cha Dar es Salaam na kusoma shahada ya ualimu akijikita katika somo la kiswahili isimu pamoja na fasihi ya Kiswahili na Kiingereza. Alifanya pia shahada ya uzamili katika masuala ya elimu hususani masuala ya uongozi na utawala chuoni hapo. Dkt Felistas alijiendeleza zaidi kitaaluma katika chuo kikuu cha Moin nchini Kenya kwa kuzama zaidi katika uwanja wa Fasihi. 


Amenifundisha somo la la lugha ya kiswahili pamoja na Kiingereza katika shule mbalimbali za msingi na sekondari nchini Tanzania kwa miaka ishirini na sita. Kwa sasa, anafundisha chuo Kikuu cha Huria cha Tanzania. 


Dkt Felistas ni mwandishi wa mashairi wa mashairi “ I wonder!”,  What a Task”, na “ The Treasure”(2005) yaliyomo ndani ya kitabu Tell Me Friends the Riddle of the Ages. kwa sasa anaandaa kitabu chake kingine kinachoitwa chake kingine kinachoitwa Siku Saba za Mwendazimu.



Mafunzo Kitabuni:


  • Mtoto mtiifu ndiye astahiliye kuigusa na kuibusu miguu ya mamaye.


  • Dunia hadaa ulimwengu shujaa.


  • Sala na kujituma katika kazi ni mhimili katika maisha.


  • Mungu huwatetea wanaosema  ukweli.


  • Njia ya mwongo ni fupi; na msema ukweli ni mpenzi wa Mungu.


  • Wadada, epuka kuwa karibu  sana vijana wasio na mapenzi mema.


  • Vijana wa kike; wajifunze ni jinsi gani wanaweza kuishi na wanaume  bila kuwaletea athari kubwa; ni vema kuwa makini na kundi la watu wenye tabia za ovyo au mtu yeyote anayekufuata kwa mambo unayohisi yatakuhatarisha usalama wako.


  • Kazi ya ualimu ni kutoa taaluma bora inayoyejenga utu bora.


  • Siku zote udongo uliopo karibu na uwaridi hunukia.


  • Aslimia kubwa ya wanaume ni walaghai.


  • Unapopata mimba hukimbiwa; mara nyingi ndio wanaoathirika , wengi huishia kufukuzwa shule na wakishajifungua huishia kukaa nyumbani.


  • Unapopatiwa fursa ya kwenda shule; usome kwa juhudi zako zote, usiingize agenda nyengine za kimapenzi.


  • Ukipoteza nafasi ya kusoma ni vigumu kuipata tena; na hata utakapoipata, utulivu wa kujisomea hautuwepo kama mwanzo kwa sababu utakuwa unawaza mtoto au baba mtoto aliyekukimbia, na kadhalika.


  • Haijalishi upo katika nyakati zipi, mwombe Mungu akutetee na kukutia nguvu.


  • Unaweza kupitia changamoto katika usomaji wako; ila katika fikra zako hizo changamoto zisikukatisha tamaa.


  • Bora umfadhili mbuzi binadamu lazima atakuudhi.


  • Jambo usililolijua ni sawa na usiku wa kiza.


  • Huwezi kutaka uheshimiwe kama hujiheshimu.


  • Baadhi ya wanaume kutembea na wanawake wengi na kuwatumia ndiyo unaume – hii ni fikra potifu.


  • Malezi ya mtoto yanahitaji ushirikano wa mzazi na walimu pamoja na mtoto mwenyewe.


  • Unaweza kuwa safari ndefu isiyokuwa na matumaini ila ni Mungu tu wa kutusaidia.


  • Sikio halipiti kichwa.


  • Mwanadamu hatabiriki.


  • Nani kama mama; wote wanaweza kukuimbia ila mama hawezi.


  • Damu nzito kuliko maji.


  • Mabananti, hamfungwi kuwa na uhusiano na wanaume kwa sababu hamuwezi kuishi katika kisiwa kisichokuwa na wanaume.


  • Dunia imeumbiwa wanawake na wanaume; hakuna mahali utaishi bila mwanaume.


  • Kitu cha msingi katika maisha ni kujitambua.


  • Unapaswa kutambua ni uhusiano upi hautakuletea athari hasi katika maisha yako.


  • Wakati ni ukuta, ukipigana nao utaumia mwenyewe.


  • Kuna ya kuchukua na ya kuacha hasa ukiona kama yatakukwamisha malengo uliyojiwekea.


  • Mnatakiwa mjue uhusiano upi ni mzuri na upi ni mbaya. Mnatakiwa mjifunze pia jinsi ya kupambana na mazingira yatakayowaingiza kwenye uhusiano mbaya.


  • Mnatakiwa pia mjue ni kipindi gani mnatakiwa kuingia kwenye uhusiano endapo muda muafaka umefika.


  • Mnatakiwa mfahamu kuwa si wanaume wote ni waaminifu; mwanaume wa uhakika kabisa  ambaye  hatakuacha kamwe ni elimu yako na kazi yako.


  • Siku zote maisha kama chanzo cha maji; jitahidini mfuate mkondo sahihi ambao hautaweza kuwapeleka pa baya – mkashindwa kufika mwisho wa safari yenu.


  • Fuateni maadili mliyoelekezwa  na wazazi na watu wenye mapenzi mema mengi. Mjitume na kuchapa kazi kwa juhudi zenu zote, na zaidi ya yote. Msisahau kumtegemea Mungu awaongoze katika yote.


  • Sikio la kufa halisikii dawa.


  • Anayeonja asali huchonga mzinga na mapenzi kikohozi; hakijifichi.


  • Haijawahi mtu akishika mambo mawili, moja lisiponyoke.


  • Mapenzi yakinoga yasiyo jali maadili ni kama ile hali ya kunguni kung’ang’ania kitanda akijua ndiyo makazi yake.


  • Usiposikiliza maonyo ya  wazazi na walezi kwa Kiburi chako, huenda hicho kiburi kikazaa shubiri na tamu uliyoifata ikawa shubiri. Na ukija shtuka ni alfajiri na wewe ndiyo unatafuta kuvuta shuka!.


  • Pamoja na sikio kutopita kichwa, wakati mwengine ni vema kusikiliza ushauri wa wadogo zetu kiumri.


  • Machozi yenu baada ya majuto hayasaidii kitu, kinachotakiwa ni kujitambua  na mabadiliko ya tabia.


  • Hakuna mchezo  wa kiume wala wa kike.


  • Ukitembea na mwizi nawe utaitwa mwizi; na siku zote kufata mkumbo katika makundi ndiyo huponza watu.


  • Maisha yatakuwa magumu tu kama utajichanganya na mambo mengine yasiyo ya msingi.


  • Kuna faida kubwa sana kutatua matatizo ukiwa katika hali ya utulivu.


  • Changamoto za maisha haziishi; kinachopaswa ni kujifunza jinsi ya kukabiliana nazo.


  • Pesa inachangia sana kuleta madhara katika dunia pale inapotumika vibaya — pesa yaweza kugeuzwa kuwa chombo cha dhuluma na ubaradhuli kwa wale wanaoitafuta.


  • Kuna baadhi wazazi wanahangaikia pesa ili wajikomboe na umaskini pamoja na watoto wao; wazazi wengine wanaharibu na kuwatumia watoto wa mwenzao katika kazi vyote pesa zao; kisha kuwaacha na umaskini wao au kuwatoa uhai wao kabisa.


  • Dunia ya sasa inaangamiza vijana wa kike na wakiume; na kushangaza zaidi, wazazi wanaoshirika katika  uumbaji wa watoto hawa, ndiyo hao hao wanaoshiriki pia katika kunyang’anya uhai wa watoto hao.


  • Ni watu wazima wenye akili timamu na pesa zao ndio wanaowatumia na kuwangamiza vijana wetu. Watu hawa hawajali thamani ya utu wa watu na hawatambui nafasi ya wazazi katika kulea vijana.


  • Jamii ina mchango mkubwa katika kumkomboa mwanamke.


  • Usikubali kumuita mtoto; mwarabu koko au mhindi koko; maana ni neno litokalo na mbwa koko, na mbwa koko ni mbwa asiyekuwa na mwenyewe.


  • Usipojifunza kutokana na yalipopita; historia huwa ina kawaida ya kujirudia.


  • Nina imani unaweza kufika mbali, mwanga mkubwa nauona mbele yako. Tumia nafasi uliyonayo, jiamini, fanyia kazi malengo yako.


  • Uwe makini na usikubali mialiko isiyokuwa na msingi hasa ile ya peke yako na iliyoko mafichoni.


  • Maisha ya ndoa yenye chembechembe nyingi za utamu zilizozamishwa kwenye  bahari ya uchungu.   


  • Kweli majuto ni mjukuu huja kinyume.


  • Usikate tamaa, fanya kazi kwa bidii huku ukimuomba Mungu akusaidie. 


  • Watoto wa kike wana hali ngumu, wako katika ulimwengu wenye ukuta wa seng’enge wale wanaowaamini na kuwategemea ndiyo wanadunga misumari; tena misumari yenye kutu.


  • Ukisimamia ukweli, utakuwa salama na haki itasimama.


  • Tupo kwenye dunia ambayo mwalimu anayetarajiwa awe rafiki, baba, mama, mlezi, kiongozi, mshauri na mwelimishaji ndiye anayemnyanyasa na  kumkandamiza mwanafunzi.


  • Naamini siyo mara zote maji ynafuata mkondo uleule, wakati mwengine yanaweza kuchepuka kwa kujitengeneza au kutengenezwa mkondo mwengine.


  • Usijutie nafsi yako, maji yakishamwagika hayazoeleki; jitahidi kwa kila uwezalo bila kujali ugumu wa utafutaji kwa kuwa mchumia juani hulia kivulini.


  • Kumbuka mtembea bure si sawa na mkaa bure, na mgagaa na upwa hali wali mkavu.


  • Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.


  • Mafanikio ya familia ni mfanikio ya wote.


  • Mwombe sana Mungu wako kwa sababu dunia hii imejaa machafuko.


  • Maisha ni bahari yenye mawimbi makali  na ndani yake, kuna papa, nyangumi, chewa na kadhalika — unatakiwa ukumbuke kuwa unaposafiri baharini unapaswa kuwa  na dira itakayokusaidia  kukwepa  misukosuko.


  • Kuwa makini katika kubaini yupi rafiki na yupi mnafiki.


  • Unaweza kunyang’anywa mali lakini huwezi kunyanganywa kilicho kichwani mwako.


  • Fanya kazi halali na kujituma bila kujali jinsi yako ili uweze kupata mafanikio na kuweza kujitegemea.


  • Biashara haina undugu, Inahitaji umakini, kujituma, ubunifu na nidhamu ya hali ya juu.


  • Wanawake wengi wana hadithi zinazofanana; na hiyo inasababishwa  na kitu ambacho kilichopo kwenye fikra za wanaume kuwa wao wana haki kuliko wanawake.





You Might Also Like

0 #type=(blogger)

Top Categories