Unamwambiaje mtu anayeongea sana apunguze kidogo bila kumfanya ajisikie vibaya?

 


Siku ya tarehe 20 mwezi wa saba nilikutana na chapisho katika mtandao wa kijamii wa X, zamani ukiitwa Twitter;chapisho hilo  likiwa limeshapishwa katika account ya  Carol Ndosi – ni dada mjasiriamali na mwanzilishi wa ‘Nyama Choma Festival’, mwazilishi mwenza wa ‘KilimoUza’ na Mkurugenzi mtendaji wa Launchpad’ likiwa linasomeka ‘Unamwambiaje mtu anayeongea sanaaaa apunguze kidogo bila kumfanya ajisikie vibaya?’ 


Chapisho hilo likafanya nipate takafuri na kunifanya nikumbuke baadhi ya makala, mahojiano ya watu mahiri katika nyanja tofauti katika maisha, nukuu, na vitabu vya maendeleo binafsi kuhusu umuhimu wa kusikiliza sana na kuzungumza kidogo! Kwa bahati iliyo mbaya watu wengi katika medani tofauti tupo mbioni kila uchwao, kwenye kujinoa na kujiimarisha katika ujuzi na tabia nyingine za kutuletea mafanikio binafsi na za kijamii ila tunasahau kwa kiasi kikubwa kujiimarisha katika ujuzi hadimu na adhimu wa kusikiliza wengine.


Sijui ni ubinafsi, au sijui ni kitu gani kinachotufanya kuwapa nafasi wengine ya kutusikiliza kuliko tunavyopaswa sisi kuwa sikiliza wao, hata kama ni wao wamekuja kwetu kwa ajili ya sisi kuwasikiliza, ndoto, maono, tabu, mahangaiko yao na mambo mengine mbalimbali ya kimaisha, kikazi hata ya  kiimani — Ila tunabaki kuwa wazungumzaji kana kwamba tunajua wanayoyapitia vichwani,maishani au katika fuad zao.


Hii tabia kusema la ukweli inakera sana na inaumiza kwa sababu inafanya tusiweze kuwaelewa watu, kwa kupenda kwetu kuongea au kuzungumza sana. Mahali ambapo tiba ilikuwa ni kuwapa usikivu wetu.


Najua sio dada Carol Ndosi tu limemkuta hili, hata mimi na wewe tushawahi kupitia  nyakati kama hizo; ambazo unahitaji usikivu wa mtu ili utue mzigo mzito uliomo mtimani au kichwani mwako ila unaishia kukwazika.


Kwanini hapo mwanzo nilisema kusikiliza ni ujuzi? kwa sababu sasa dunia yetu ina wasikiaji na wazungumzaji wengi ila tuna uhaba wasikilizaji wachache kama vile mvua katika jangwa la  Sahara. ndiomana siyo ajabu sasa hivi, katika semina mbalimbali, mafundisho na ujuzi huu unafundishwa na kuhimizwa kwa watu ili waweze kuwa walezi, wazazi, walimu na viongozi mahiri na hodari; samabamba na tabia ya kujisomea vitabu na madodoso yenye taarifa sahihi kama vile tafiti nk.


Najua huenda fuadini au kichwani mwako unaweza kupata mawazo ya kuwa ni vizuri kujizungumzia, ni vizuri kuyasema mawazo yetu. Ni kweli upo sahihi ila “vikizidi sana ni mno” cha mbilecho cha bibi yangu asemavyo! Naamini dada Carol ameshindwa kuvumilia na kumfanya kuomba ushauri wa kupata njia bora ya kumuambia mtu huyo roporopo bila kumkwaza aliyopo katika mzunguko wake, huenda ni wa kikazi au wa karibu zaidi.


Au hujui ile kanuni ya mawasiliano ya 80/20; kuwa kwenye kuwasiliana na watu na kuchangamana na watu — asilimia 20; zungumza. Na asilimia 80; sikiliza na siyo usikie. Mana kuna tofauti kubwa kati ya kusikiliza na kusikia; kusikia ni desturi ya viumbe – kusikia ni kutafsiri kile kilichosemwa. Lakini kusikiliza ni sanaa ya kusikia maneno sanjari na kuhisi hisia za mwengine zinazobebwa katika maneno yao; kuvaa viatu vyao; kusoma lugha yake ya mwili mana hapo ndipo unakamilisha sanaa ya usikilizaji. Maana kwenye lugha ya mwili inaweza kusema hapana ila mdomo wa msemaji umetamka ndiyo – wale wanaofanya kazi ya upelelezi na kuhoji watuhumiwa wanakijua hiki ninachokizungumza.

 

Soma zaidi: “Usirithi adui wa mtu” – Dkt Jakaya Kikwete


Au je, unajua kwanini Mola Jalia ametuumba kuwa na mdomo mmoja na masikio mawili? Mimi nadhani anataka tuwe tunasikiliza sana na kuongea kidogo. Maana hakuna aliyewahi kujifunza kitu kipya kwa kuzungumza ila wapo wengi wanajifunza kwa kusikiliza. Ukiwa unazungumza hua unaongea yale unayoyajua tu. ila ukiwa msikilizaji unapata kujifunza yale uliyo kuwa unayoyajua na usiyoyajua. Na hoja hiyo inapigiliwa msumari katika kichwa chako isikutoke abadan kwa nukuu hii aliyosema Mtakatifu Seraphim wa Sarov “ Kuwa kimya sana, zungumza kidogo - na utulivu utakuja moyoni mwako, na roho yako itakuwa na utulivu na amani.”


Je huu msemo wahenga unaosema  “ Samaki afunguaye mdomo wake ndiyo hunaswa na ndoano.” pia hausadiki? Kuwa kuna hekima na busara kwenye uzungumzaji kidogo na kusikiliza sana? Au ile picha inaonesha mnyama mwenye mdomo mrefu ukiwa umenasa katika pacha za ngazi akiwa anajitahidi kwenda juu huku msanifu ikisindikizwa na maneno nayosomeka ‘ kinacho kukwamisha usikifikie malengo yako ni mdomo wako – haujawahi kukutana nayo kwenye mitandao ya kijamii? hii si kiroho tu kwamba utaita ni husda, kwenye mafundisho ya dini yanatuasa kuwa “usiri una baraka” maana kwa mdomo wako unaweza kutoa taarifa ambazo watesi wako wakazitumia kukwamisha yote kwa uongeaji wako usio na tija na kutaka kuonekana unajua kumbe ndiyo unajiangamiza.


Ndiomana Dale carnigie alipata  kusema “Kuacha wengine wazungumze inasaidia katika ustawi mzuri wa kifamilia sajjari na ustawi wa kibiashara.”


Mwanafalsafa wa ufaransa aliwahi patakusema “"Ukitaka maadui, wapite marafiki zako; lakini ukitaka marafiki, waache marafiki zako wakupite." Hii ni kweli kwa sababu marafiki zetu wanapotuona wanatupita wanajihisi muhimu; lakini tunapowapita, wao - au angalau baadhi yao - watajihisi duni na kuwa na wivu hiyo inakwenda sambamba ukitaka kuzungumza na kujizumgumzia sana… ila binadamu, hahaha! Dunia simama nishuke miye! 



Ngoja nikuibie siri ndugu yangu; viongozi wakubwa wengi wanaosifiwa kama viongozi bora, mahiri na  hodari ukiacha tabia na juhudi zao nyingi wana tabia  hizi mbili zinazofanana. Mosi ni tabia ya kupenda kusoma vitabu na pili kusikiliza sana. Na mimi leo nipo hapa kukuibia tabia hii ya pili ya kusikiliza; kwa kukutajia viongozi na baadhi za aya katika vitabu kuhusu swala hilo ili kuchokwa na kukera watu katika mazungumzo iwe ni historia ila kikubwa naomba usikaze tu fuvu lako na ukubali kubadilika baada ya hapa:


Soma Zaidi: Billionaire under construction; Expand your mind, enlarge your thinking


Tukianza na viongozi; Mfano bora wa muda wote ambao mpaka naandika makala hii tunajaivunia nao ni Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton ambaye kwa kipindi chote akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu. ametajwa kuwa ni mtu mahiri katika kuwasiliana na watu kwa muda wote duniani; na pia umahiri wake wa kusikiliza ni mfano mkubwa wa kuigwa licha ya kuwa pia ni mzungumzaji mzuri ila sifa hii yake ya usikivu ndiyo inayozumgumziwa sana. Na hawa ni baadhi ya viongozi wakinukuliwa wakimuuelezea umahiri  Bill Clinton katika kusikiliza;

(Bill Clinton) photo credit: Getty Images/ CBS photo archive


  • “Clinton alikuwa na kipaji cha kipekee cha kusikiliza kwa makini na kuelewa mawazo na hisia za watu. Alijua jinsi ya kuunganisha na kila mtu, bila kujali walikotoka au walichokuwa wanakabiliwa nacho.” — Tony Blair

  •  “Bill ana uwezo wa ajabu wa kuingia ndani ya akili na hisia za mtu mwingine. Anaweza kusikiliza kwa makini sana na kujua kinachoendelea katika maisha ya mtu huyo. Hii ni moja ya sababu kuu za mafanikio yake ya kisiasa.” – Hillary Clinton

  • "Clinton alikuwa na uwezo wa kumsikiliza mtu na kumfanya ahisi kuwa yeye ndiye mtu muhimu zaidi katika chumba hicho. Hii ilimsaidia sana katika kujenga mahusiano na kuleta mabadiliko." —  Al Gore

  • "Niliona jinsi Clinton alivyoweza kusikiliza kwa makini sana katika mikutano ya kimataifa. Alifanya kila mtu ajisikie kuwa maoni yake ni muhimu na kwamba alichukua muda kuelewa kila mtazamo kabla ya kutoa uamuzi." Madeleine Albright

Na viongozi wengine ambao ni mahiri na kusikilza ambapo ujuzi huo umewafanya kuwa miongoni mwa viongozi bora waliowahi kupata kuishi katika  sayari hii ambayo siye tunaiita Dunia; viongozi hao ni 


  • Barack Obama  –  (“Obama ana uwezo wa kipekee wa kusikiliza kwa makini na kuelewa hisia na mawazo ya watu. Hii inamfanya kuwa kiongozi mzuri na mwenye huruma.” - Michelle Obama), 


  • Dalai Lama – (Dalai Lama ana uwezo wa ajabu wa kusikiliza na kuonyesha huruma kwa kila mtu anaye kutana naye. Anawawezesha watu kuzungumza kwa uhuru na kueleza hisia zao.” - Richard Gere), 


  • Nelson Mandela  – ("Mandela alikuwa na uwezo wa ajabu wa kusikiliza na kuelewa maoni ya watu wengine, hata kama hawakukubaliana naye." - Desmond Tutu), 


  • Abraham Lincoln – (“Lincoln alijua jinsi ya kusikiliza watu kwa makini, na alitumia maoni yao kusaidia katika kufanya maamuzi bora zaidi.” - Doris Kearns Goodwin),  na


  •  Angela Merkel – (“Merkel ni kiongozi anayejua kusikiliza na kuchukua muda kufikiria kabla ya kutoa maamuzi. Hii inafanya kazi yake kuwa yenye ufanisi zaidi.” - Barack Obama).


Bila kusahau nchi yetu ya Tanzania; baadhi ya viongozi wanaoingia katika orodha hii ya wasikilizaji wazuri na mahiri ni Rais mstaafu wa awamu ya nne; Dkt. Jakaya Kikwete na Mtaasisi ambaye kwa sasa ni marehemu, Bw. Ruge Mutahaba aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Clouds Media Group na mwanzilishi mwenza wa Tanzania House of Talent(THT).

Rais Kikwete na Ruge Mutahaba


Kwenye mahojiano yake katika kipindi cha ‘Salama Na’ aliyekuwa msaidizi wa kuandika hotuba za Rais kikwete kwa muda wa miaka miwili na Msaidizi wake binafsi kwa miaka nane, ambaye kwa sasa ni  Balozi wa nchi yetu  katika nchi ya  Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini, Mhe. Togolani Mavura;alipoulizwa swali hili na Salama Jabir, “ What a kind of person his?” akasema “ Mtu mwema sana, mtu rahimu sana, mtu mlezi sana, mtu anayefanya ujisikie raha kufanya naye kazi… anasikiliza sana, kupita kiasi na pia ni mtu makini sana…” hii inaonesha ni kwa jinsi gani Rais wetu ni msikivu na si mara ya kwanza watu waliobahatika kufanya kazi naye kwa karibu kukiri tunu hii aliyekuwa nayo.


 Kwa upande wa Ruge Mutahaba – tunakuja kwenye siku ya kupewa heshima zake za mwisho katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam. katika watu walio bahatika kumuuelezea kwa jinsi gani walivyokuwa wana mfahamu marehwmu Ruge Mutahaba: alikuwa ni Maznat kama anavyofahamika na watu wengi japo sio jina lake halisi; Maznat ni mmiliki wa ‘Maznat Bridal’, na chuo cha ujasiriamali na urembo kijulikanavyo kama ‘Maznat Beautyl and entrepreneurship’ yeye alimuelezea Ruge kama ifuatavyo kuhusu kusikiliza: ... unajua mimi nilikuwa nafikiria Ruge ni mtu mkubwa, na muona kwenye TV, namuona everywhere nikajua nikifika pale, akiniuliza swali nitaongea kidogo na yeye ataendelea kuongea. Lahasha! Alinyamaza kimya! Nilijielezea akatulia. Nahisi kwa mara ya kwanza maishani mwangu nilijua kama nasikilizwa; nilistaajabu! Kwamba kuna watu wanasikiliza kiasi hicho. Akanisikiliza ; akatabasamu…” 


Na mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mstaafu  ( kipindi hicho alikuwa Waziri wa Muungano na Mazingira chini ya ofisi ya Makamo wa Rais) na pia ni Mbunge wa jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, Mhe January Makamba yeye katika hotuba yake alisema mengi ila mimi nanukuu hiki kipande “... kuna habari imetolewa hapa kwamba anasikiliza, kweli na mimi nimeshuhudia. Ukikaa na Ruge ukizungumza unaweza usimuamini kwamba kuna mtu mwengine yeyote duniani anapata attention kama unayopata wewe. Na hilo ni somo kubwa sana alinifundisha. Mimi kama mwanasiasa mara nyingi, tayari tuna mawazo mtu akifungua tu, tayari una majibu! Na subira ya kusikiliza ni somo kubwa ambalo amenipa na nitamkosa sana kwa ajili hiyo…



Na ushuhuda wa tatu ni kutoka kwa mwandishi wa habari maarufu katika kipindi cha asubuhi cha redio kiitwacho ‘Power Breakfast’ kinachoruka hewani na kituo cha Clouds FM, Cza katika uzinduzi wa Ruge Mutahaba Foundation tarehe 26 ya mwezi sita, mwaka 2022 , nayo ni baada ya miaka mitatu baada ya kifo cha Ruge. Cza ni kijana ambaye alikutana na marehemu Ruge kipindi anasoma akiwa yupo kidato cha tano na  kufanya kazi kwa takribani miaka nane  –  kwa sasa  Cza ni meneja wa Ubunifu na Biashara wa Clouds Media Group; na hivi ndivyo alivyo muelezea “ … la pili kuhusu Ruge kuwa kiongozi, ni mtu ambaye alikuwa anasikiliza sana na mtu ye yote ambaye amefanya kazi na Ruge atakubaliana na mimi. Kwamba ni mtu msikivu sana kwa sababu aliamini kwamba; kwamba msingi wa mawazo makubwa ni kusikiliza.”

 


Sasa twende kwenye vitabu baada ya kumaliza kwenye viongozi,na kwenye vitabu tutakiangalia kitabu kiitwacho “ How to Win friends and Influence People” cha mwandishi Dale Carnegie; moja ya mwandishi nguli katika masuala ya maendeleo binafsi, hotuba za hadhara na mawasiliano ya ufanisi. Katika sehemu ya tatu, sura ya sita katika hiki kitabu “ Dale anaanza kwa kuandika "Watu wengi wanaojaribu kuwashawishi wengine kwa njia yao ya kufikiri kwa kuongea sana wenyewe. Waache watu wengine wazungumze. Wanajua zaidi kuhusu biashara zao na matatizo kuliko wewe. Kwa hiyo, waulize maswali. Waache wakueleze mambo kadhaa.

Ikiwa hukubaliani nao unaweza kushawishika kuingilia kati. Lakini usifanye hivyo. Ni hatari. Hawatakusikiliza wakati bado wana mawazo mengi yanayohitaji kuelezea." 


Soma Zaidi: One Hour to Live, One Hour to Love; The True Story of the Best Gift Ever Given


Katika mifano aliyoitoa ni mfano wa mwakilishi wa Kampuni ya uzalishaji wa vitambaa vya samani za magani G.B.R; changamoto iliyomkuta ya kutoweza kuongea wakati uwasilishaji wa kampuni yake – na kufanya asaidiwe na Rais wake, yeye akawa anaitikia kwa kichwa, kutabasamu tu. yeye anakiri Rais wake alielezea zaidi kuliko vile alivyofanya hii ikafanya kampuni yake kupata kandarasi ya dola za kimarekani millioni moja na laki sita. Na mfano mwingine ni  mzazi ambaye alimtaja kama Bi. Wilson, ambaye alikuwa hafurahishwi na tabia ya mwanae Laurie, ambaye alikuwa hana utii mbele yake, alikuwa mtu wa kutoka tu kwenda kumuona rafiki yake wa kike na kila mara akiwa akirudi kwa rafiki yake anamfokea, yeye Bi. Wilson anasema alikuwa ameshamfokea zaidi ya mara elfu kumi. Kwa mara zote hizo bado kijana alikuwa kichwa ngumu, kama wasemavyo ndugu zetu wa Kenya. Ila mambo yote yalibadilika siku ambayo Laurie aliporudi, Bi. Wilson alitamani kumfokea ila alijizuia kumkaripia  na kubaki kumuangalia Laurie, na kumuuliza “Kwanini Laurie?’ … Laurie baada ya kujua hali ya mama yake, alimuuliza “unataka kujua?” Bi. Wilson alitikisa kichwa kuonesha ishara ya kuwa anataka kujua, japo Laurie alionesha kusita ila alifanikiwa na kumuueleza mama yake –   Bi. Wilson alikiri kuwa siku zote hizo alikuwa hajawahi kumsikiliza mwanaye, zaidi ya kumpa maagizo afanye hiki, asifanye hiki — akawa bibi mkubwa badala ya kuwa msiri wake.


Mpaka hapa tumeshaona uzuri na faida ya kuwa wasikilizaji bora; sasa tukirudi  katika swali aliotupa Carol jinsi ya kupata njia bora ya kuwaambia watu wetu wakaribu, wafanyakazi wezetu ambao wanapenda sana kuongea. Kwa watu waliotoa majibu katika chapisho ni zaidi ya  machapisho  75 yameshapishwa mpaka naandika makala hii. Na hayo yafuatayo ni miongoni mwa machapisho waliochangia katika  chapisho hilo:


  • “Mwambie we unaakili sana na upo positive sana,nitachukua yote uliyoyasema.Nipe kwa hatua Ili niyafanyie kazi,yakiwa mengi yatanishinda.Halafu mshukuru,muage na ondoka,au omba udhuru” — @Kanali23

  • "Aisee maongezi yetu mimi nawe hatumalizi saa hii, naomba nifanye shughuli kidogo nitakurejea " onyesha kuwa interested and engaged… Hakikisha unampigia tena.” — @SincerelyBiseko

  • “By the way, kuongea sana ni matokeo ya kutaka kusikilizwa au kutojiamini. Take them out of their misery by asking simple but clear questions itasaidia kumfanya ajiskie unamuamini na unamuelewa na upo interested na monologue yake”. —  @Sonic563

  • "Wisdom has bee chasing you but you have always been faster." —  Abdulrazack972

  • “Muulize: Hivi ulishawayi kufikiliya kwanini una masikio mawili na mdomo mmoja” — @RealFelixManzi

  • Kaa kimya mpaka atakapoacha kuongea na usiongee neno lolote akiwa anaongea...ww sikiliza weeeeeeeeeeee” — @MawazoMataje

  • “ 'Lips zako zinapendeza sana ukiwa umefunga mdomo' – mwambie hivyo kama ni mpenzi wako lakini.” —  @bongolyrix

  • “Unamuangalia tu, unamsikiliza bila reaction, don't nod or shake your head...don't show any sign of validation or rejection just be silent and look them in the eye. It will be very uncomfortable and they might even ask am I talking too much? … Akimaliza change the subject.” — @BrendahPeace

Nami sikuishia hapo ikabidi  nikauulize watu wangu wa karibu, jamaa na rafiki kuhusu hili swali baadhi ya majibu yalinifurahisha na kunifikirisha kwa mitazamo yao ila nadhani ni bora kuwashirikisha na nyie majibu haya manne yaliyonivutia zaidi:


  • “Kama tumezoeana. Mi namwambia kabisa unapendeza zaidi ukiwa na maneno machache japo kuongea sana nayo ni vizuri ila kwa wewe ukipunguza. Au maintain kiwango hichi hapo poa kabisa! Japo kuna wale watu ukimwambia ukweli anaweza kukuchukia(mithali 9:8) —  so apo kuna mawili nikiona vipi naweza mwacha tu kama haina madhara yoyote ya ye kuongea sana — Au kama sioni shida kumsikia ila nIkiona too much naweza angalia na mood yake afu tunaongea ila asilimia kubwa naangalia ye ni mtu wa aina gani ndo nimwambie au nimwache tu.”– Flora

  • “Kwanini asijiskie vibaya wakati ongea yake ina nifanya me nijisikie vibaya, long story short normally sipendi ku-respond mtu akiwa talkative namuacha tu aongee, the best response is NO RESPONSE” –  Yaah Makai

  • “Ningemwambia punguza kuongea....kama ni mwanangu sana ningemalizia unaboa!” – Rosemary

  • “Tumiaa lugha kwa  ufasaha, Mdomo huumba” – Nourat Jinyevu


Soma Zaidi: Gu Family Book


Nami tafiti yangu nimekuja na majibu sita ya kumuambia mzungumzaji sana. Japo Kumwambia mtu anayezungumza sana apunguze kuongea bila kumfanya ajisikie vibaya inaweza kuwa ni  changamoto, lakini inawezekana kwa kutumia njia sahihi na yenye heshima, yenye uungwana bila kutweza utu na hadhi yake; mbele yako ama mbele ya kadamnasi. Na haya ni majibu natumai yanaweza kupokwa na mtu anayeongea sana bila kujisikia vibaya

  • "Samahani, ninafurahia mazungumzo yetu lakini ningependa tuweze kutoa nafasi kwa wengine pia kushiriki mazungumzo haya."

  • "Ninaona kama kuna mambo mengi ambayo napenda kushiriki pia, na ningependa pia kusikia kutoka kwa wengine."

  • "Naona tunapata mazungumzo mazuri, lakini pia ningependa kumsikia [jina la mtu mwingine] kuhusu hili."

  • "Nadhani itakuwa vizuri kama kila mmoja wetu atapata nafasi ya kuchangia mawazo yake ili tupate mtazamo wa kila upande."

  • "Nafurahia sana mazungumzo yako, lakini naona kama umenipa kazi ya kuwa msikilizaji tu leo!"

  • "Kwa kuwa muda wetu ni mfupi, labda tunaweza kutoa nafasi kwa kila mmoja kutoa mchango wake kwa ufupi."

Kama bado unang’ang’ania eti sijui ni hulka yako; vikaenda vikarudi; sasa hii ni dawa yako chungu kumeza na kunywa

  • Mosi, chanzo kikubwa cha misala mingi unayokutana nayo ni kwa ajili ya kuongea sana.

  • Pili, asilimia 90 ya watu wanaingia kwenye matatizo au kukosa wanavyovitaka kwa kuongea sana.

  • Tatu, unawahi kuchokwa sana kwasababu unaongea sana!

  • Na mwisho asilimia 90 ya matatizo yanatokana kuongea.

Kuwa mskilizaji mzuri! Mruhusu mtu mwingine azungumze zaidi wakati wa mazungumzo. Maana uzungumzaji kidogo katika mazungumzo unakufanya usikike zaidi kulliko ukiwa chiriku.



Kusoma Zaidi.



You Might Also Like

0 #type=(blogger)

Top Categories