Adili na Nduguze.

 


Kuhusu Kitabu

Adili na Nduguze ni riwaya ya Sheikh Shaaban Robert inayozungumzia jinsi ambavyo Adili, kijana mwenye roho na tabia njema, alivyohusudiwa na ndugu zake (Hasidi na Mwivu), walimchukia na kumpatia mateso na kumweka katika hali ngumu katika nyakati tofauti.


Nduguze walimtesa kiasi cha kutosha na kama malipo ya makosa yao wakageuzwa manyani na jini liitwalo Huria. Lakini kwa moyo wake mwema, Adili akayaombea msamaha baada ya miaka mingi yakitunzwa naye kwa mateso ya kuyapiga kiboko kila usiku na kuyapa posho.


Baada ya hapo, Huria alikubali pendekezo la Adili na wakarejea katika utu tena. Mara baada ya baba yao kufariki dunia, Adili na nduguze waligawana mali sawa kwa sawa katika sehemu tatu.


Kwa sehemu kubwa, kitabu cha ‘Adili na Nduguze’ kimefanana na kitabu cha kwanza cha ‘Alfu Lela U Lela.’


Kuhusu Mwandishi

Sheikh Shaaban Bin Robert, pia anajulikana kama Shaaban Robert (1 Januari 1909 – 20 Juni 1962), alikuwa mshairi, mwandishi, na mwandishi wa insha kutoka Tanzania ambaye alitetea uhifadhi wa mila za ushairi wa Tanzania. Robert anasherehekewa kama mmoja wa wanafikra, wasomi, na waandishi wakubwa wa Kiswahili kutoka Tanzania katika Afrika Mashariki na ametajwa kama "Mshairi mkuu wa Kiswahili" na pia anajulikana kama "Baba wa Kiswahili." Pia anaheshimiwa kama mshairi wa kitaifa.


Shaaban alizaliwa kwa baba mwenye asili ya Wayao na mama mwenye asili ya Kidigo katika kijiji cha Vibamba, kata ya Tangasisi, wilaya ya Tanga, iliyoko kusini mwa Jiji la Tanga katika Mkoa wa Tanga, Tanzania (wakati huo ikiitwa Afrika Mashariki ya Kijerumani). Jina la Robert ni jina la afisa wa kikoloni wa Kiingereza aliyemwomba mzazi wake kumpa jina hilo. Kwa hivyo, kwa maana halisi, Robert lilikuwa jina lake la pili (siyo jina la ukoo au jina la mwisho), jina lake la kwanza likiwa ni Shaaban. Shaaban mwenyewe kwa muda fulani aliandika jina hilo kama 'Roberts' badala ya 'Robert'. Kuanzia mwaka 1922 hadi 1926 alisoma jijini Dar es Salaam, na akawa wa pili katika darasa la wanafunzi 11 na kupokea Cheti cha Kuondoka Shuleni chini ya mfumo wa elimu wa kikoloni wa Kiingereza wakati huo katika Tanganyika.


Baada ya kupokea cheti cha shule, Shaaban alifanya kazi katika nyadhifa mbalimbali kama mtumishi wa serikali ya kikoloni. Kuanzia mwaka 1926 hadi 1944, alifanya kazi kama afisa wa forodha katika maeneo tofauti ndani ya eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kituo kimoja katika Kisiwa cha Kwale, wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani wa sasa. Kuanzia 1944 hadi 1946 alifanya kazi katika Idara ya Wanyamapori. Kuanzia 1946 hadi 1952 alifanya kazi katika Ofisi ya Wilaya ya Tanga, na kutoka 1952 hadi 1960 alikuwa katika Ofisi ya Upimaji huko Tanga. Alifanya kazi kwa ukaribu sana na Chama cha TANU na Julius Nyerere. Matukio mengi ya uzoefu wake wa utumishi wa umma yameingizwa katika maandiko yake. Katika maisha yake, alipokea Tuzo na Medali ya Margaret Wrong kwa Fasihi ya Afrika na aliheshimiwa na serikali ya Uingereza kwa kutunukiwa cheo cha Mwanachama wa Order ya Uingereza (M.B.E.).


Robert alichangia katika kuendeleza lugha ya Kiswahili na mapambano ya kuheshimu utu wa binadamu. Alikuwa mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu. Alipigania uhuru na usawa wa kijinsia, na alipinga ubaguzi wa rangi na dini nchini Tanzania. Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, alimvutia sana marehemu Shaaban Robert, na alithamini na kuendeleza sana kazi zake za kiakili. Shaaban pia aliwaheshimu kwa usawa Waislamu na Wakristo. Hii inaonekana katika majina yake mawili yasiyo ya kawaida (Shaaban—jina la Kiislamu na Robert, jina la Kikristo). [Jina la Robert kwa hakika lilikuwa moja ya majina kadhaa ya baba yake, mengine yakiwa Selemani na Ufukwe.]


Sheikh Shaaban Robert alifanikiwa kuandika insha, vitabu, nathari, na mashairi, na baadhi ya maandiko yake ni sehemu ya mtaala wa shule na vitabu vya kusomwa katika elimu ya juu.


Kwa ujumla Shaaban Robert aliandika vitabu ishirini na nne. Baadhi ya vitabu hivi ni: Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Maisha Yangu Baada ya Miaka Hamsini, Utubora Mkulima. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha ya Kichina, Kiingereza na Kirusi


Mafunzo Kitabuni


  • Tendo hukidhi haja maridhawa kuliko neno.

  • Haja ikishughulikiwa kwa matendo hupatikana upesi, lakini ikishughulikiwa kwa maneno huchelewa kama sadaka.

  • Ukamilifu wa mtu duniani ni tabia njema.

  • Kila mtu bora, anatakiwa kuonyesha ubora wake kwa kuchukuana na watu.

  • Hulka njema sawa na mali.

  • Waungwana hawanyimai neni lisilokalifu.

  • Hapana roho mbinguni wala duniani isiyopitiwa na majuto.

  • Hiari na dhima ni mambo mawili ambayo hayatimiziki kwa wakati mmoja.

  • Hapana mtu awezae kwenda njia mbili kwa wakati mmoja.

  • Ukali wa mbwa hutokana na msasi.

  • Waungwana hawasemi uongo.

  • Busara kubwa kichwani  haina faida kama moyoni hamna chembe ya wema.

  • Maisha ni safari, na dunia ni matembezi kwa wanadamu – maskani yao ya milele yako peponi.

  • Hapana mtu ambaye atabaki duniani.

  • Mwana wa mhunzi asiposana huvukuta.

  • Mali bila daftari hupotea bila habari.

  • Hakika mtu anayehesabu mapato na matumizi yake yake hafi maskini.

  • Mtu hushindwa kujua pato lake mwenyewe huonyesha uchache wa uangalifu.

  • Mali hufidia roho, lakini roho haifidiwi na kitu.

  • Moyo hauhimili mshawasha wa mfululizo; hasa mshawasha wenyewe ukitokana na mtu anayempenda  au tamaa ya utajiri.

  • Mwanadamu ameumbwa kwa heri na shari; Hasa kwa heri.

  • Lugha ni pingamizi kubwa kwa watu duniani.

  • Kula uhondo kwataka matendo; asiye matendo hula uvundo.

  • Tamaa ya mali ni kubwa; mioyo mingi haitoshewi na mali; walakini, kwa kweli fikira ya mali isiyo kadiri ni mzigo usio chukulika.

  • Nusu ya hasara ya mwanadamu hutokea kwa sababu wenyewe hawataki kutumia vipawa vyote walivyopewa.

  • Onyo la bure likikataliwa huleta majuto ya milele.

  • Turufu humwenda kwa mchezaji siku zote.

  • Kuna mambo yanayofaa na yasiyofaa ushirika; ndoa ni moja ya jambo lisilofaa ushirika.

  • Ushirika katika ndoa unapasa wanayama na ndege.

  • Mwanaume hakukusudiwa kwa fahali wa kila mtamba, wala mwanamke kuwa tembe la kila jogoo.

  • Mawazo mabaya hurusha usingizi

  • Kutazama hatari usoni kunavunja moyo wa mtu.

  • Wanauma waninda mbaya ufisadi unapo wapofusha.

  • Kilio cha kujisingizia hakina machozi wala matanga.

  • Asiyefurahia heri ya mwenziwe, shari yake kumhadhibikia.

  • Atakae makaa ya mgomba hapati kitu ila jivu tupu.

  • Bahari haiweki amana na kitu kieleacho kwa kuwa alielea aliokoka.

  • Mwanadamu haishiwi na uchafu kama kilihafu.

  • Hapana mtu mwema aliyetayari kuungama kwa makusudi aadhibiwe; wala mtu asiyejisingiziaa wema makusidi asiadhibiwe.

  • Bila ujasiri nadra mtu kafanikiwa

  • Mwenye saburi hukidhiwa haja zake.

  • Neno takatifu gumu kufahamika, lakini linatija kwa wajisumbuao kulifasiri.



Umbuji wa Shabaan Robert ulionikosha katika kitabu hiki

“Ilikuwa si desturi ya Rai kusema maneno na kuacha wengine watende maneno, lakini alifanya matendo akaacha watu wengine waseme maneno.”


“Salama ya maisha yao ilikuwa bora kuliko faida iliyopotea umaskini umetengana hatua moja tu  na utajiri.”


“Kama uzuri ulio peponi wamejaliwa malaika, karibu uzuri wote ulio duniani alijaliwa msichana huyo. Uzuri wake ulikuwa haalingani na uzuri wa mwanamke yeyote aliosifiwa kuwa mzuri katika zama zake… matamko yake yalikuwa kama mafuatano ya muziki.”


“Moyo wa Adili ulitekwa na mapenzi ya tamasha hiyo. Akili yake ilipotea na nuru ya macho yake ilizimika kitambo ila ilikuwa mara ya kwanza mshale wa mapenzi kupenya moyoni mwake. ulipenya katikati ya moyo wake.”


“Kila tendo jema au baya ni mfano kwa raia wake. Kwa sababu ya maisha ya milele ibada ya mizimu ilikuwa maangamizi na uimamu wa ukwabwere ujinga mtupu.”


“Hapana jibu la haraka. Tumia wakati upendao wa kufikiri nimesema neno la Mungu. Mungu hachelei tisho la mwanadamu, kazi ya mikono yake mwenyewe neno takatifu. Neno takatifu gumu kufahamika, lakini linatija kwa wajisumbuao kulifasiri.”


“Hunde alikuwa kiumbe cha mwisho katika wanaume walikuwa na sura mbaya… alikuwa hatazamiki kwa ubaya, licha ya yeye kumtazama mtu.”


“Wanawake hukutana na mikasa mingi mibaya duniani. Mioyo yao huelemea na haja zisizokubalika; masikio yao hutuwa  uziwi kwa maombi ya baraka, na miili yao ni mawindo ya jeuri daima.”


“Malkia wa Majini alitabasamu akasema, “ usiseme kikembe mwanangu. Wema wako ulikuwa asilia, nawe ulitangulia kuutenda; na wa binti yangu ulikuwa wa kuigiza, nae ametenda nyuma. Asili na uijagi ni vitu mbalimbali. Havilingani wala havitalinganika milele.”


“… katika ini alifumwa na mshale, na moyoni mwake mishono ya maumivu makali.”


“Tazama adhama na tabia ya Adili. Alikuwa tayari kujikalifu takalifu ilipomlazimu, kujidhabibu dhabihu ilipotakiwa; na kusamehe msamaha ilipobidi.”


“Alipogeuka kwa ndugu zake Adili , Rai alionya, kama wavivu walijitahidi kuwa hodari; ilikuwa kinyume hodari kuwa mvivu; kama waovu walitaka kuwa wema, ilichukiza wema kuwa wovu; kama masikini walitafuta  utajiri; ilikuwa ujinga matajiri kufuja walichokuwa nacho; kama mbegu iliongezwa mchanga, ilikuwa harabu mtu kuwa ndugu yake; pia ilikuwa aibu kubwa sana kwa wazuri kutenda maovu.”


“Aha, ilikuwa furaha kubwa ilioje! Mioyo miwili  ya mapeni iliyopoteana ilikutana tena. Neno halikuwezekana kusemeka. Walitazama wakichekana. Walishikana mikono wakabusiana. Walikuwa katika siku bora ya maisha yao.”


    Tenzi

Tenzi #1


Miguu ya msichana, Na mwendo alikwenda,

Adili alipoona moyo wake ulimshinda.

Alikuwa na miguu mfano wa charahani,

Wala ulimwengu huu, hajatokea kifani,

Alipendeza hatua wakati alipokwenda,

Chini viatu chalia, mithali kama kinanda.

Alikwenda kwa madaha, mwanamke mwenye enzi,

Yaliompa furaha kila mwenye kubarizi.


Tenzi #2


Nala sumu ndugu zangu,

Msambe naona tamu.

Takalifu kubwa kwangu,

Kuadhibu yangu damu.

Sina raha ndugu zangu,

Neno hili kwangu gumu.


Tenzi #3


Mawe huwa dhahabu,

Au jabari na chuma,

Dhambi yake hukoma.

Nishani zake thawabu,

Na heshima ya daima.


Marejeo zaidi 


  1. Shaaban bin Robert, Wikipedia, 4 February 2024

 


You Might Also Like

0 #type=(blogger)

Top Categories