Kifo Fumbo la Imani: Hadithi zote za Mapenzi lazima ziishie kwa Msiba.

Picha: Getty images/ Andrew Bret Wallis

Kifo ni fumbo la imani kama inavyopendwa kunukuliwa na viongozi wa dini: maadamu tu hai basi kufa lazima. Kifo kimeumbwa kwa ajili yetu bin Adam na kitakoma tu, pale siye wote wana wa Adamu tukiwa tumefutika katika uso wa dunia..


Tupatapo misiba huwa mara nyingi hali ya kuhamanika hutujia, mawazo na fikra mbalimbali hushamiri mpaka muda mwingine  zinatupelekea kumkufuru Mola wetu Jalia.


Hali ya kuhamanikia hutokea kwa sababu ya mshtuko mkubwa wa kihisia, huzuni kali, na maumivu ya kupoteza mtu muhimu katika maisha yetu. Hofu ya kukosa udhibiti wa hali, kutokuwa na uhakika kuhusu maisha bila wao, na upweke wa ghafla unaweza kuongezeka, na kusababisha wasiwasi uliopitiliza na kuhamanikia.  


Bi. Polina Maranova mmiliki wa Waraka wa Habari uitwayo ‘The Profile’, na pia Polina ni muandishi wa kitabu cha ‘Hidden Genius’. Katika waraka wake wa Agosti, 21 mwaka huu ulioenda  kichwa cha Waraka:  'My Annual Birthday Check-In: 11 Lessons From 33 Years on This Planet’. Katika Waraka huo allkuwa anatushirikisha mafunzo kumi na moja  ya maisha katika miaka thelathini na tatu  — kwenye funzo la sita  alizojifunza ndani ya miongo mitatu ni kuwa: “Hadithi zote za mapenzi zimetarajiwa kumalizika kwa msiba  (Tragic loss).” kwenye kulichambua funzo la maisha alisema alishawahi  kumsikia mwandishi Nicholas Sparks (ni muandishi gwiji wa riwaya kubwa nne ambazo anaelezea misiba mizito (Tragic loss) ya visa vya mapenzi; The Notebook, A Walk to Remember, Dear John, na A Message in a Bottle)  akisema haya kwenye mahojiano:


"Kwangu, mapenzi na msiba vimeungana. Huwezi kuwa na moja bila jingine. Na kadiri mapenzi yanavyokuwa makubwa, ndivyo msiba unavyokuwa mkubwa zaidi.”


"Unaona, kila siku mamilioni na mamilioni ya watu ulimwenguni wanakufa, na sisi sote tunaendelea na maisha yetu, tunakwenda kazini, hatujali. Lakini pale inapokuwa ni mtu unayempenda — dada yako, mke wako, babu au nyanya yako, rafiki yako — ni kama dunia yako inaanguka. Na kadiri mapenzi yalivyokuwa makubwa, ndivyo msiba unavyokuwa mkubwa zaidi.


"Hivyo basi, kwa tafsiri, hadithi zote za mapenzi lazima ziishie kwa msiba."’


Nazidi kujazia nyama kwenye mantiki hiyo ya ‘hadithi zote za mapenzi lazima ziishie kwenye hali ya msiba’. Kwahiyo  ilimradi tu kuna upendo, hakutakosa kuwa na huzuni. Huzuni ya wakati uliopita; ya maisha kuendelea na ombwe la nafasi tupu ambalo zamani lilijaa vicheko, furaha, kuthaminiana, amani na nguvu za watu tuliowapenda.


Kwenye upendo uliokithiri wa ndugu, jamaa, wenzi na rafiki unaweza kumithililisha  na bustani yenye maua ya aina nyingi. Upendo wa watu wa karibu ni kama miti yenye mizizi imara, inayotupa kivuli na utulivu, ikitufanya tuhisi tuna ulinzi na msaada wa kudumu. Upendo wa wenzi ni kama waridi wenye harufu nzuri na rangi angavu, unaotuletea furaha ya kipekee, shauku, na utamu wa mapenzi. Upendo wa marafiki ni kama maua ya porini yanayochanua kila kona, yakijaza bustani yetu na rangi za furaha, kicheko, na urafiki wa kweli. Bustani hii ya upendo ina aina mbalimbali za uzuri, kila moja ikiongeza thamani ya kipekee na kutufanya tuhisi tumezungukwa na furaha, nguvu, na upendo usio na mipaka. Na siku tukiwapoteza ni huzuni kubwa sana  kama mti mkubwa ulio kwenye uwanda mkavu, ukiwa umesimama peke yake. Mizizi yake inajitahidi kufikia maji ya kumbukumbu, lakini udongo wa upweke hauna rutuba. Majani yamekauka, na kila tawi lililokatika ni kama upotevu mwingine, huku mti ukisimama peke yake, ukijaribu kuishi licha ya maumivu hayo yote ni kwa sababu huzuni ni mwendelezo wa kawaida wa upendo.


Huzuni ni taa kubwa ya neon, yenye mwanga mkali inayoonekana kila mahali, ikionyesha kila sehemu, ikitangaza kwa sauti kubwa, 'Upendo ulikuwa hapa.' na kwa maandishi madogo,'Upendo bado upo'.


Ndugu yangu hakika msiba usikie kwa jirani ila  usiombae ukufike;  maana ni afadhali kusikia juu ya matatizo au misiba inayowapata watu wengine (jirani), lakini unapaswa kuomba na kutarajia kwamba misiba hiyo isikufike au isikupate wewe mwenyewe.


Japo muda mwengine huo msemo unaokena una ukakasi ila naamini unatoa wito mkubwa wa kuwa na huruma na kuelewa maumivu ya wengine wakati huo ukitamani na kuomba kwamba wewe mwenyewe usipatwe na hali kama hiyo. Hii inaonyesha ukweli kwamba msiba ni kitu kibaya,kinaumiza sana ila kwa waamini tunajua ndiyo njia ya kukutana na Mola wetu Jalia na ingawa tunaweza kushiriki huzuni na wengine, ni jambo ambalo hakuna mtu anayetamani kumkuta. Bora uwe kwenye nafasi ya kufariji kuliko kufarijiwa; unayetoa kuliko kupokea.

Ila kama tujuavyo, Mola wetu sio utaratibu wake – na hafanyi kama fahamu za binadamu zinavyotaka; siku zote humuita yeyote anayemtaka; hajali mdogo wa rika au mkubwa wa rika; Rais au raia; tajiri au masikini; fukarafuke au hoehae; una kaa Masaki au Madongoporomoka; mnyonge au jasiri – yeye akikutaka atakuita tu.



Soma: Unamuambiaje mtu anayependa kuongea sana, apunguze kuongea



Basi nasi tukiwa hatuko tayari jambo hili zito kutufika. Ghafla mgeni alikuja kama kimbunga cha hisia, kilichoturudisha nyuma kwa mshangao na maumivu. Kila neno lililotamkwa lilikuwa na uzito mkubwa, likitupatia taarifa mbaya ambayo hatukuweza kuamini. Ilikuwa ni kama dunia yetu ilivunjika, na ghafla tukaingia katika giza la huzuni na mashaka, huku tukijaribu kuelewa jinsi hiyo ilivyotokea: basi mbawa za kaka wa rafiki yangu kipenzi zilikuwa tayari kwa ajili ya kwenda kuonana na Mungu wetu – aliyetupa  yeye; nasi tukamuita kaka. Ikiwa sisi fuad zetu haziko tayari. Kilicho baki ni  majonzi na simanzi katika mitima yetu. Nyuso zetu zikagubikwa na huzuni, miili yetu ikaingia hali ya uyabisi kama umuonavyo panya akiwa amemwagiwa maji.


Ila kama tunavyojua kuwa hakuna anayeweza kuzuia kadari ya Mungu, ndipo nikiwa katika dimbwi la mawazo, nikiajribu kuvaa viatu vya rafiki yangu ila nikajikuta vinanipwaya tu, ndipo ule msemo usemao “tutegemea mambo mazuri na yakutufurahisha, ila huku tukijiandaa na mambo mabaya ambayo huenda ya kutuhuzunisha na kutuumiza.” hapo nilipopata wazo la kuandika makala hii ya jinsi ya kujiandaa na kuweza kuikabiri huzuni ya kuwapoteza watu wetu wa karibu: ndugu, wenzi, watoto, wafanyakazi wenzetu n.k.


Jinsi ya kukabiri huzuni ya kupoteza mtu wa karibu


Kupitia uzoefu wa kumpoteza mpendwa wako yeyote kunaweza kuwa na uchungu sana kwa watu.


Kwa hivyo, leo nataka kukushirikisha  ushauri ambao nimeupata kutoka kwa Buddha ambao utakusaidia kutuliza hisia zako na kukusaidia kukabiliana na huzuni hii ya kumpoteza mpendwa.


Kabla hatujaendelea mbele Buddha ni nani? Buddha ni jina alilopewa Siddhartha Gautama, mwanzilishi wa dini ya Ubuddha. Alikuwa mwana wa kifalme aliyezaliwa karibu na mwaka 563 KK katika mji wa Lumbini, ambao sasa ni sehemu ya Nepal. Baada ya kuona mateso ya maisha—ugonjwa, uzee, na kifo—aliamua kuacha maisha ya anasa na kuanza safari ya kiroho ili kutafuta suluhisho la mateso ya binadamu.


Baada ya miaka mingi ya tafakari na majaribio ya maisha ya kujinyima, Siddhartha alipata mwanga chini ya mti wa Bodhi na kuwa Buddha, yaani aliyeamka. Mafundisho yake makuu yanahusu ‘Ukweli minne ya Ukuu’, ambao unaeleza kuhusu mateso ya maisha, chanzo chake, na njia ya kuyaepuka kupitia ‘Njia ya Nane’.

Buddha; Buddhism
Picha kwa hisani: getty images/halepak



Moja ya nukuu zake maarufu ni: "Afadhali usitafakari kama vile ndoto, badala yake tafakari kama vile maisha yako yanavyokuwepo."


Buddha anachukuliwa kuwa mwalimu mkubwa wa kiroho na mawazo yake yameathiri maisha ya watu wengi, na wafuasi zaidi ya millioni 520 kwa kutoa njia ya utulivu wa ndani na ukombozi wa kiroho – na huyo ndiyo Buddha.


Turejee kwenye mada yetu: Haijalishi kama wewe ni mwanaume, mwanamke, mtawa, muamonaki au mtu wa kawaida kama wewe. Yeyote yule unayeweza kuwa, fikiri kwamba kuna  siku moja lazima nitatenganishwa na watu wote ninaowapenda na vitu vyote ninavyovipenda. Huu ndio ukweli.


Sasa, huu ndio ukweli mchungu; na uchungu huo unatokana na sisi  tuweze kukubali ukweli, kwa maana kikawaida hatupendi kukubali ukweli. Watu hukimbia kutoka kwenye ukweli ambao hawapendi kufikiria kama watafariki siku moja. Hawapendi kufikiria kwamba watazeeka siku moja, hawapendi kufikiria kwamba wataugua au kupata magonjwa siku moja, ama kutengana na marafiki zetu wa muda mrefu.


Kwa hivyo, hayo yote ndio ukweli wa maisha haya. Katika maisha yetu hapa duniani, sote tunapaswa kujua na kukabiliana na ukweli huu kuwa: kifo, ugonjwa, uzee, na kumpoteza mpendwa tumeumbiwa navyo.


Huu ni ukweli ambao hatuwezi kuuzuia;hapana, huwezi kuuzuia: siwezi kuuzuia, na hakuna anayeweza kuuzuia hapa duniani visitutokee.


Kwa hivyo, jambo moja ambalo Buddha anatufundisha ni "kukubali ukweli, uone ukweli kama ulivyo na ujaribu kufikiria juu yake. Na kuchukulia ulivyo na si kama tunavyotaka uwe. Tujue kuwa kuna siku moja lazima nitenganishwe na watu hawa wote walio karibu nami."




Soma: An Hour to Live, an  Hour to Love



Kuna watu wengi sana ni wa karibu na tunawapenda sana. Ukweli ni kwamba siku moja mimi na wewe lazima tutenganishwe na watu hawa wote sasa au tutawalazimisha, au tutawaacha. Kwa hivyo, Buddha anasema jiandae kukabiliana na ukweli huu.


Unawezaje kujiandaa kukabiliana na ukweli huu? Kwa kufikiria juu yake kila siku. Buddha alisema "fikiri mara kwa mara lazima nitatenganishwa na watu hawa walio karibu nami, siku moja, huo ndio ukweli."


Unapofikiria kuhusu hili, kuna faida nyingine kubwa ya kufikiria hivi. Ni ipi hiyo? Unapofikiria kuhusu hili! Unaweza kuonyesha upendo wako na huruma yako kwa dhati, kwa nini? Kwa sababu unajua kwamba hutakuwa karibu nao kwa muda mrefu.


Unajua kwamba hutakuwa nao milele. Unapojua hilo na unapojua kwamba una muda mfupi kuwa na watu hawa walio karibu nawe, basi unaweza kuonyesha huruma yako, upendo wako, na kuwajali kwa kiwango kikubwa zaidi katika muda huu mfupi. Utafanya bidii na kujihimu kuwaonyesha upendo na huruma yako.


Kwa hivyo, kuanzia sasa na kuendelea, jiandae kukabiliana na ukweli huu. Unapojiandaa kwa hilo, unapokutana na hali hizi katika maisha halisi, unaweza kukabiliana nazo kwa akili thabiti.


Wakati mwingi watu hukutana na hali hizi bila mafanikio. Mara nyingi huhisi huzuni kubwa na huzunika sana wakati mwingine. Watu wengine hujitoa uhai.


Unapoufanya moyo wako uwe tayari kukabiliana na ukweli, unapoufanya moyo wako kuwa na nguvu ya kutosha kukabiliana na ukweli, unaweza kuendelea na maisha yako na unaweza kukabiliana na huzuni hiyo kwa mafanikio.


Fikiria juu ya ukweli, usiukimbie, kisha utaweza kuunda akili yenye furaha na amani katika maisha yako.”


Nicholas Sparks
Photo credit: Getty images/D-Kein
Maombolezo:

Sasa kama inavyo fahimika siye binadamu ni viumbe vya hisia na wala si viumbe wa kimantiki katika upokeaji wa mambo na vitu hasa katika mambo mazito kama vile msiba na vya kutuhuzunisha; hata nami kutokana na msiba huu mzito ulitufikia, uliofanya tumehamanike; tukakosa utulivu wa mwili na akili ila Mola pekee ndiye wa kutuvusha katka hili – wa kutupa mioyo subra, ustamihilivu, uvumulivu.


Ukweli ni kwamba, machozi yalitutoka mengi sana yakatosa macho, nyuso na zetu fuad. Yalikuwa hayazuiliki sababu pigo zito liliotujia likalegeza sukurubu za milazimu yake yote. 


Maana mauti yake ya mapema yalikuwa ni msiba na hasara kubwa sana kwetu. Kama viumbe wenye mioyo yenye nyama tulishindwa kujizuia. Machozi yalitirirka kama maji katika mahali wazi. Sheikh Shabaan Robert alipata kusema: “Machozi tumeumbwa nayo katika miili yetu na kumwagika kwake… ni wajibu kwa wanadamu.”


Kama ile methali isemayo: aliyekosa titi la mama la mbwa huamwa – nikajiunga na  familia kuhuzunika na kuomboleza pamoja nao. Basi kwenye kutaka  kujifariji nikaenda kuupitia ushairi wa Sheikh Shabaan Robert alioandika kama kuomboleza baada ya kupata msiba mzito wa mkewe Bi. Amina; ambao kichwa cha shairi hilo aliliita ‘Amina’ – Basi nami likawa chachu ya kuandika shairi hili la ‘kakae” kwa kaka yetu mpendwa ambaye Mola muumba kwa uweza wake usiyo na shaka aliyemtwaa siku chache katika maisha yetu. Japo nimetumia baadhi ya maneno katika shairi la ‘Amina’ la sheikh Shabaan Robert yote ni katika kujifariji miye na familia katika msiba huu. 

 


Soma: Adili na Nduguze 



Kakae

 Kakae umejitenga, kufa umetangulia,

Kama ua umefunga, badala ya kuchanua,

Nakuombea mwanga, peponi kukubaliwa,

Umeniacha nalia, Muumba akupokee.


Nilitaka unyanyuke, kwa kukuombea dua,

Sikupenda ushindike, maradhi kukuchukua,

Ila kwa rehema yake, Mungu amekuchagua,

Umeniacha nalia, Muumba akupokee.


Majonzi hayaneneki, kile nikikumbukia,

Nawaza kile na hiki, naona kama ruia,

Mauti siyasadiki, kuwa mwisho wa dunia,

Umeniacha nalia, Muumba akupokee.


Nasadiki haziozi, roho hazitapotea,

Twafuata wokozi, kwa mauti kutajia,

Kaka yangu kipenzi, peponi utaingia,

Umeniacha nalia, Muumba akupokee.


Jambo moja nakumbuka, sahihi ninalijua,

Kuwa sasa umefika, ta’bu isikosumbua,

Japo nimehamanika, nyuma nilikobakia,

Umeniacha nalia, Muumba akupokee.



Nihitimishe kwa kumbushana nafsi zenu na yangu  kuwa: Katika safari ya mwanadamu hapa duniani, kifo ni hakika isiyoweza kuepukwa. Qur'an inatufundisha: "Kila nafsi itaonja mauti, na kwa hakika mtapewa kikamilifu malipo yenu Siku ya Kiyama" (Surah Al-Imran, 3:185). Hii ni hatima ambayo wanadamu wote tutaipitia, tukikumbushwa kuwa maisha ya sasa ni ya mpito kuelekea maisha ya milele. Ni jukumu letu kuwataja kwa wema waliotangulia mbele ya haki, kuwaombea rehema na maghfira, tukimwomba Mwenyezi Mungu awasamehe madhambi yao, na awape makazi ya amani katika bustani za Peponi.


Kama Mtume Muhammad (S.A.W.) alivyosema: “Kaburi ni bustani katika mabustani ya Peponi au shimo katika mashimo ya moto wa Jahanamu.” (Hadith, Tirmidhi), tunamwomba Mwenyezi Mungu awajaalie makaburi yao kuwa kama viwanja vya bustani za Peponi. Na zaidi ya hayo, tunamwomba Mwenyezi Mungu awape vitabu vyao kwa mkono wa kulia siku ya Kiyama, kama anavyosema: "Na ama yule atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: 'Haya, someni kitabu changu! Hakika nilijua kuwa nitakutana na hesabu yangu'." (Surah Al-Haaqqa, 69:19-20).


Maandiko ya Biblia pia yanathibitisha kuwa kifo ni sehemu ya mpango wa Mungu, na ni njia ya kuingia katika uzima wa milele. Biblia inasema: "Kwa kuwa Mungu alimpenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele."(Yohana 3:16). Huu ni uthibitisho wa upendo wa Mungu kwa wanadamu, na ahadi ya wokovu kupitia imani. Pia, katika kitabu cha Ufunuo, tunapata tumaini la uzima wa milele: "Nao watamsujudia Yeye aliye juu ya kiti cha enzi, nao wataishi milele na milele." (Ufunuo 22:3-5). Hii ni ahadi ya uzima wa milele kwa wale waliookolewa na waliotenda haki.


Kwa pamoja, tunamwomba Mwenyezi Mungu, na kwa Wakristo pia wakimwomba Mungu kupitia Yesu Kristo, awaweke ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki, katika amani, awape makazi ya amani ya milele katika Pepo Daraja la Juu, Jannatul Firdaus, na siku ya mwisho wapokewe kwa mikono ya kulia kama ishara ya ushindi. Hili ndilo tumaini letu kuu, kwamba hatimaye tutakuwa na furaha ya milele, kama ilivyoahidiwa katika vitabu vitakatifu. Amina.







You Might Also Like

0 #type=(blogger)

Top Categories